Mkongwe wa muziki wa dansi nchini Tanzania Muhidin Gurumo wa bendi ya Msondo Ngoma ametangaza uamuzi wake wa kustaafu kufanya muziki alioutumikia kwa miaka 53.
Gurumo (73) aliitoa taarifa hiyo jana (August 22) alipozungumza na waandishi wa habari kwenye
Ukumbi wa Habari Maelezo, Dar es Salaam huku akizitaja sababu mbili za uamuzi huo, kwa mujibu wa Mwananchi.
Sababu ya kwanza aliyoitoa Gurumo ni swala la umri wake kuwa umeenda, lakini pia ameamua kuwapa nafasi vijana kuendeleza muziki pale alipouachia. Pia aliongezea sababu nyingine ya kifamilia na kudai kuwa kwa miaka yote hiyo mke wake alikuwa anakosa nafasi ya kuwa naye kutokana na kurudi usiku wa manane kutoka kazini.
Pia amesema kutokana na umri alionao, imekuwa vigumu kwake kwenda sambamba na kasi, mabadiliko na mahitaji mapya ya muziki huo, hivyo kazi hiyo amewaachia vijana. “Muziki umekuwa asili yangu kwa muda mrefu, sasa naamua kustaafu ili kutoa fursa kwa vijana kuendelea kupiga muziki huu”. Mkongwe huyo aliongeza kuwa pamoja na kwamba amestaafu kuimba lakini ataendelea kuwa mshauri kwa wanamuziki vijana wanaouendeleza muziki.
Bendi alizowahi kuzitumikia ni pamoja na Kili Chacha, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, DDC Mlimani, Safari Sound na Msondo Ngoma.
No comments:
Post a Comment